Aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
ALIYEKUWA Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amemshukuru Rais John Magufuli kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kumsaidia katika kipindi chake cha mpito huku akisisitiza kwamba, atashirikiana na aliyeshika wadhifa huo, John Kijazi kujenga Tanzania mpya.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi, Kijazi, aliyeapishwa jana, alisema ataendeleza jitihada za Rais Magufuli kutumbua majipu, ikiwa ni moja ya njia ya kurejesha nidhamu kwa watumishi wa umma na Serikali kwa ujumla.
Viongozi hao walitoa kauli hizo jana Ikulu, Dar es Salaam, wakati wakizungumza na waandishi wa habari baada ya Rais Magufuli kumwapisha Kijazi kushika Ukatibu Mkuu Kiongozi.
Sefue: Nimeheshimika Balozi Sefue ambaye alishiriki katika kumuapisha Dk Kijazi ikiwa ni ishara ya kumkabidhi wadhifa huo, alimshukuru Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kwa kumpatia fursa ya kuwatumikia wananchi na kumteua kushika wadhifa huo aliouhitimisha rasmi jana.
Aidha, alimshukuru Dk Magufuli kwa kumpatia nafasi ya kuendelea kumsaidia mara baada ya kuchaguliwa na Watanzania kuwaongoza katika kipindi chote cha takribani miezi mitatu.
“Namshukuru Rais Magufuli kwa kuniamini, haikuwa lazima kwake kuendelea na mimi lakini aliamua kuwa nami katika kipindi chake cha mpito ili niweze kumsaidia. Nashukuru sana najisikia nimeheshimika kuwa pembeni yake kwa kipindi chote hicho,” alisema Balozi Sefue.
Alimpongeza Dk Kijazi kwa kumpokea kijiti cha wadhifa huo wa Ukatibu Mkuu Kiongozi, akimuahidi kumpatia ushirikiano na ushauri atakapohitajika.
“Nampongeza sana mwenzangu kupatiwa fursa hii, naamini awamu hii ya tano, kutokana na utendaji wake inaashiria mambo makubwa katika nchi yetu, naahidi kumpatia kila aina ya msaada mimi pamoja na makatibu wakuu viongozi waliomaliza muda wao kwa faida ya nchi yetu,” alisisitiza.
Kasi ya Kijazi Kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Kijazi, alisema dhana ya utumbuaji majipu maana yake ni kujenga nidhamu ndani ya Serikali kwa kuhakikisha maeneo yote yenye kasoro yanarekebishwa.
“Nitamsaidia Rais katika kufanikisha hili kwa sababu katika moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja na suala zima la mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa,” alisisitiza Dk Kijazi.
Alisema pamoja na kipaumbele hicho cha kupambana na rushwa, pia Serikali imeweka mkazo katika eneo la kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato, hali ambayo itasaidia kuongeza pato la taifa na hivyo kutoa huduma bora kwa wananchi.
Alisema ili nchi yoyote iendelee kiuchumi na maendeleo hayo yafikie wananchi wake, ni lazima ijikite katika kukusanya mapato yake ya ndani.
Alisema akiwa kiongozi na mtumishi mkuu wa Serikali, atahakikisha anaendana na kasi ya utendaji ya awamu ya tano katika kusimamia na kutekeleza kwa vitendo vipaumbele hivyo kwa ajili ya kuboresha uchumi wa nchi .
Alisema atasimamia pia kujenga utumishi uliotukuka, wenye tija na nidhamu. “Namshukuru Mungu kutokana na uteuzi huu lakini pia namshukuru mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kunipa kazi hii kubwa.
Kwa kuwa mimi ndiye mtendaji mkuu serikalini, nitawajibika na kuwa kiungo kikubwa kati ya Rais na wizara pamoja na idara zake,” alisema Balozi Kijazi.
Alisema kwa mujibu wa majukumu ya kazi yake, anapaswa kufahamu kila wizara inafanya nini na kumjulisha Rais juu ya hali ya utumishi, mazingira ya watumishi pamoja na mwenendo wa nidhamu zao.
Alisema katika kutekeleza majukumu ya Baraza la Mawaziri ambalo naye ni mjumbe kutokana na wadhifa wake huo, ni jukumu lake kusimamia utekelezaji wa uamuzi unaofikiwa.
“Nafahamu kuwa katika kutekeleza majukumu yote haya siwezi kufanya peke yangu. Kwa kuwa kila wizara ina mtendaji mkuu nitafanya nao kazi kwa ukaribu ili kujua yale yanayohitaji usimamizi na uamuzi ili kwa pamoja tufikie lengo la kuwatumikia wananchi,” alisema.
Wasifu wa Kijazi Kabla ya uteuzi huo, Balozi Kijazi alikuwa mwakilishi wa Tanzania nchini India, Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal makazi yake yakiwa jijini New Delhi, India kuanzia mwaka 2007 na hivyo kumfanya kuwa Mkuu wa Mabalozi wote wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi.
Amekuwa Mkuu wa Mabalozi wa Afrika nchini India huku akitajwa kuwa mtetezi mkuu wa wanafunzi wenye asili ya Kiafrika nchini humo.
Kabla ya kuwa balozi, Kijazi alikuwa Katibu Mkuu , Wizara ya Ujenzi na baadaye Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu kuanzia mwaka 2002 hadi 2006, kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hatimaye kupangiwa kituo cha New Delhi, India.
Kati ya mwaka 1996 hadi 2002, alikuwa Mhandisi Mwandamizi wa Ujenzi wa Barabara ndani ya Wizara ya Ujenzi kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Barabara za Mikoa ndani ya Wizara hiyo hiyo.
Dk Kijazi alipata Shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa Umma mwaka 1982 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara Kuu kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza mwaka 1992. Katibu Mkuu Kiongozi Kijazi, ana mke, Fransiscar Kijazi na wamejaliwa watoto watatu; David, Emmanuel na Richard Kijazi.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameagana na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) anayemaliza muda wake, Joyce Mends-Cole, Ikulu jijini Dar es Salaam. Pamoja mambo mengine, alimshukuru kwa kazi kubwa ya kuhudumia wakimbizi kwa kipindi chote alichokuwepo nchini.
Kwa upande wake, Cole alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri inayofanywa na Tanzania kusaidia nchi zenye matatizo, hususan migogoro ya kisiasa ambayo husababisha watu wake kuwa wakimbizi.
Pia amepongeza kuteuliwa kwa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, kusaidia usuluhishi wa mgogoro wa Burundi ambao umesababisha idadi kubwa ya wakimbizi kukimbilia Tanzania.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment