Mar 15, 2016

Ansarullah: Tuko tayari kwa mazungumzo ya amani

Ansarullah: Tuko tayari kwa mazungumzo ya amani
Harakati ya Ansarullah ya Yemen imetangaza kuwa iko tayari kufanya mazungumzo ya amani ili kuhitimisha mashambulio ya kivamizi ya Saudia dhidi ya ardhi ya Yemen.

Saleh As-Samad, mkuu wa tawi la kisiasa la harakati ya Ansarullah ameeleza kupitia taarifa kwamba harakati hiyo itakaribisha maelewano au hatua yoyote itakayowezesha kukomeshwa uvamizi dhidi ya ardhi ya Yemen.

Akiashiria ubadilishanaji mateka uliofanywa baina ya Ansarullah na Saudia, As-Samad amesema hatua hiyo ni sehemu ya utangulizi wa mazungumzo na kwamba ikiwa viongozi wa Saudia wataonesha nia ya kutaka kuhitimisha uvamizi huo kunaweza kuwepo matumaini ya kuchukuliwa hatua nyengine kwa ajili ya kufikia amani.

Wiki iliyopita, harakati ya Ansarullah ilimwachia huru askari mmoja wa Saudia mkabala wa kuachiliwa Wayemeni saba. 

Ubadilishanaji huo wa mateka ulifanyika kwa usuluhishi wa viongozi wa makabila ya Yemen na kwa lengo la kupunguza machafuko katika maeneo ya mpakani na kurahisisha ufikishaji misaada ya kibinadamu kwa wananchi wa Yemen.

Wiki iliyopita pia wawakilishi wa Ansarullah walielekea Riyadh, Saudi Arabia kwa mazungumzo kuhusiana na usitishaji mapigano katika eneo lote la mpaka wa pamoja wa nchi mbili. 

Safari hiyo ilifanyika tarehe 7 Machi kwa mwaliko wa viongozi wa Saudia baada ya wiki moja ya mazungumzo ya siri.

0 comments:

Post a Comment