Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka
(MSF) limetangaza kuwa, wakimbizi wa Kiislamu katika Jamhuri ya Afrika
ya Kati wanakabiliwa na hali mbaya.
Ripoti ya shirika hilo imebainisha
kwamba, maelfu ya wakimbizi wa Kiislamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati
wanaishi katika mazingira magumu na mabaya sana baada ya kuyakimbia
makazi yao wakihofia usalama wa maisha yao.
Shirika la Madaktari Wasio
na Mipaka limetangaza kuwa, wengi wa Waislamu hao wamelazimika
kuyakimbia makazi yao kutokana na kuandamwa na mashambulio ya wanamgambo
wa Kikristo wa Anti-Balaka.
Shirika hilo limeeleza kuwa, zaidi ya watu
laki tano wanaishi katika hali mbaya kwenye kambi za wakimbizi zilizoko
katika nchi za Chad, Cameroon, Jamhuri ya Kongo Brazzaville na Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo.
Inaelezwa kuwa, serikali ya nchi hiyo haina
uwezo wa kudhibiti usalama wa Bangui, mji mkuu wa nchi hiyo na hata
katika baadhi ya mikoa ya nchi hiyo. Aidha habari kutoka Bangui, mji
mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati zinasema kuwa, hali ya usalama katika
mji huo bado haijaboreka licha ya kuweko juhudi za kila upande.
0 comments:
Post a Comment