Waziri wa zamani wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mansour Yusuph Himid amekamatwa na
Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume na sheria
imefahamika visiwani humo jana.
Mansour ambaye alivuliwa uanachama wa CCM na
kupoteza nafasi ya mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la
Kiembesamaki, alikamatwa nyumbani kwake huko Chukwani na kufanyiwa
upekuzi mkali na askari wa kikosi cha upelelezi wakiongozwa na Naibu
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao
makuu ya Jeshi hilo, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai
Zanzibar Salum Msangi alisema Jeshi la Polisi lilipokea taarifa za
kiintelejensia kuwa waziri huyo wa zamani anamiliki silaha kinyume na
sheria.
Msangi alisema mara baada ya kupokea taarifa hiyo,
Jeshi hilo lilianza kuifanyia kazi na jana ilikuwa siku rasmi ya kwenda
kufanya upekuzi ndani ya nyumba yake na kufanikiwa kupata silaha aina
ya Shortgun yenye namba za usajili 1904136413 aina ya Bore Browning
pamoja na risasi 112.
Msangi alisema kwa mujibu wa sheria ya umiliki wa
silaha, hairuhusiwi kumiliki zaidi ya risasi 55 kwa silaha aina ya
Shortgun na kueleza kuwa Jeshi hilo linaendelea kumhoji waziri huyo wa
zamani.
Vilevile, Msangi aliongeza kuwa silaha nyingine
aliyokamatwa nayo ni bastola yenye namba F76172W pamoja na risasi 295
jambo ambalo ni kinyume na sheria ya umiliki wa silaha za moto, ambapo
mmiliki anatakiwa kuwa na risasi zisizozidi 25.
“Tunafanya uchunguzi ili kujua ilikuwaje amiliki
kiwango kikubwa cha risasi, pamoja na kumiliki silaha aina ya bastola
kinyume na sheria ya Zanzibar inayokataza watu binafsi kumiliki silaha
za moto.
Upekuzi huo ambao ulifanyika chini ya ulinzi mkali
wa polisi saa saba za mchana ulichukua saa zipatazo mbili na baadaye
waziri huyo wa zamani alifikishwa katika Makao Makuu ya Polisi kabla ya
kuhamishiwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi
Madema kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano.
Mansour alipakiwa katika gari aina ya Toyota
Landcruiser, iliyokuwa ikisindikizwa na gari nyingine ya Polisi
iliyokuwa na askari wa FFU, wakiwa na silaha.
Mara baada ya kufikishwa Makao Makuu ya Polisi,
baadhi ya ndugu wakiwamo watoto wa Rais mstaafu wa Zanzibar, akiwamo
Fatma Karume ambaye ni mwanasheria pamoja na mdogo wake Abeid Amani
Karume ambao walikuwa wakifuatilia hatua zote zilizokuwa zikichukuliwa
na Jeshi hilo.
“Mimi ni mwanasheria naomba kuwepo hatua zote za
mazungumzo” alisema Fatma Karume muda mfupi baada ya waziri huyo wa
zamani kuchukuliwa kwa ajili ya kufikishwa katika kituo cha Polisi
Madema.
Vitu vingine vilivyokamatwa na Jeshi hilo ni
pamoja na kompyuta mpakato (laptop) na vifaa vingine vya mawasiliano
ambavyo vyote vinaendelea kufanyiwa uchunguzi.
0 comments:
Post a Comment