Kiongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar
(Jumiki), Sheikh Farid Hadi Ahmed (43) na mwenzake Jamal Nooridin
Swalehe (38), wameunganishwa na watu wengine 18 wanaoshtakiwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka manne likiwamo
la kula njama ya kuingiza watu nchini kushiriki katika vitendo vya
ugaidi.
Pia, wanakabiliwa na shitaka la kuwaingiza watu nchini kushiriki katika
vitendo vya ugaidi, kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo hivyo.
Mawakili wa Serikali, Peter Njike, Bernard Kongola na George Barasa
wakiwasomea hati ya mashtaka hayo yanayowakabili washtakiwa hao walidai
kuwa Sheikh Farid ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mbuyuni, Zanzibar
na Fundi Ujenzi, mkazi wa Koani Zanzibar, Swalehe walijihusisha na
makosa hayo ya ugaidi kinyume na Kifungu cha 27(c) cha Sheria ya Kuzuia
Ugaidi ya 2002.
Mbali na Farid na Jamal, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na mashtaka
hayo ni Nassoro Hamad, Hassan Bakari, Ahtari Humoud, Mohamed Isihaka,
Abdallah Hassan, Hussein Mohamed, Juma Sadala, Said Kassim, Hamis Amour,
Abubakar Abdallah, Salum Ali, Salum Amour, Alawi Othuman, Rashid Ally,
Amir Hamis, Kassim Salum na Said Shehe.
Walidai kuwa kati ya Januari 2013 na Juni mwaka huu washtakiwa hao kwa
pamoja walipanga njama ya kutenda makosa hayo ya kula njama za kusaidia
na kuwezesha kufanyika vitendo vya kigaidi.
Njike alidai kuwa katika kipindi hicho na maeneo tofauti nchini, Sheikh
Farid aliwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary nchini ili kushiriki
kutenda makosa ya ugaidi.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu
chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo
hadi Mahakama Kuu.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine.
Hakimu Hellen Liwa aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 20, mwaka huu na
kuamuru washtakiwa kupelekwa rumande kwa sababu mashtaka yanayowakabili
ni miongoni mwa mashtaka yasiyo na dhamana.
Baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili, Sheikh Farid alidai
mahakamani hapo kuwa anashangazwa na kitendo cha wao kukamatwa Zanzibar
na kushtakiwa Tanzania Bara wakati hawana ndugu, baba wala mama katika
upande huo wa Jamhuri ya Muungano.
“Tunashangaa kushtakiwa huku Tanganyika wakati Zanzibar ni nchi yenye
Mwanasheria Mkuu, Jaji Mkuu na askari watiifu tu na kila kitu,” alisema
na kuongeza kuwa wamekamatwa Aprili lakini hadi sasa upelelezi bado
haujakamilika na kuhoji ni upelelezi gani huo.
0 comments:
Post a Comment