Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa hivi
karibuni na Taasisi ya Twaweza umebainisha kuwa wananchi wanaunga mkono
kwa kiwango kikubwa Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Ripoti ya utafiti huo uliofanyika Februari, mwaka huu kwa njia ya
simu za mkononi na watu kuulizwa kuhusu mchakato wa Katiba, inaeleza
kuwa kama wananchi wangeipigia kura rasimu hiyo mwezi huo, Katiba hiyo
ingepitishwa kwa asilimia 65 Zanzibar na asilimia 62 Tanzania Bara.
Akiwasilisha ripoti hiyo jana, Mtafiti wa Twaweza, Elvis Mushi
alisema kati ya watu waliohojiwa upande wa Tanzania Bara, asilimia 20
wangepiga kura ya hapana, kwa upande wa Zanzibar watu ambao wangesema
hapana wangekuwa asilimia 19.
“Watu ambao walisema hawana uhakika na hawajui lolote kwa upande wa
Zanzibar ni asilimia 19 na Tanzania Bara asilimia 15,” alisema.
“Zaidi ya asilimia 60 ya wapiga kura kutoka Tanzania Bara na Zanzibar
walisema wana nia ya kupiga kura ya kuikubali Katiba (rasimu) kama
ilivyo sasa.”
Muundo wa Serikali
Kuhusu muundo wa Serikali, Mushi alisema: “Asilimia 80 ya Wazanzibari
wanaunga mkono muundo wa serikali tatu. Kwa Tanzania Bara wanaounga
mkono serikali tatu ni asilimia 43.”
Alisema takwimu hizo ni tofauti na zilizotolewa miezi minane
iliyopita ilipotolewa Rasimu ya Kwanza ya Katiba, ambayo asilimia 51 ya
wananchi wa Tanzania Bara walipendekeza muundo wa serikali tatu.
Alisema baada ya kutolewa kwa Rasimu mbili za Katiba (ya kwanza na ya
pili), Wazanzibari wanataka uhuru zaidi wa kujitawala au muungano wa
serikali tatu, huku wananchi kutoka Tanzania Bara wakigawanyika nusu kwa
nusu juu ya muundo wa serikali wanaoutaka.
Mafuta na gesi
Kuhusu mafuta na gesi kutokuwa masuala ya muungano, bali chini ya
mamlaka ya Serikali za Tanganyika na Zanzibar, Mushi alisema suala hilo
lilikubaliwa na wananchi wa Tanzania Bara kwa asilimia 42 na Zanzibar
asilimia 74.
Alisema Watanzania sita kati ya 10 (asilimia 60) wanaosikiliza
mjadala kuhusu Rasimu ya Katiba, wanawaamini wabunge kuwa wanawakilisha
masilahi yao bungeni, wanaunga mkono uwazi na uwajibikaji kama
ilivyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba.
Mambo mengine ambayo yameungwa mkono na wananchi ni utaratibu wa
kudhibiti na kuwawajibisha wabunge, uwepo wa mgombea binafsi na mgawanyo
wa madaraka.
Utafiti huo umefanyika huku kukiwa na mvutano mkali katika Bunge
Maalumu la Katiba kuhusu muundo wa muungano na kusababisha wajumbe wa
Bunge hilo wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
kususia kutokana na CCM kuunga mkono muundo wa serikali mbili ambao ni
tofauti na Rasimu ya Katiba iliyopendekeza muundo wa serikali tatu.
Mushi alisema maoni ya wananchi ni muhimu yakazingatiwa bila kujali
nini kinaamuriwa na wawakilishi kwenye Bunge la Katiba, kwa sababu
baadaye watapiga kura ya maoni kupitisha Katiba.
Maoni ya kwanza ya utafiti huo yalikusanywa Tanzania Bara kati ya
Februari 12 na Machi 4, mwaka huu na taasisi hiyo ilipata majibu ya kaya
1,547 na mengine yalikusanywa kati ya Julai 16 na Julai 30 mwaka jana
na kaya 1,708 zilitoa majibu.
“Kwa upande wa Zanzibar, utafiti kwa kutumia simu ya mkononi
ulifanyika Februari 24 na Machi Mosi, mwaka huu na kaya 445 zilitoa
majibu,” alisema
Apr 25, 2014
Asilimia 80 ya Wazanzibari wanaunga mkono serikali tatu:UTAFITI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment