Dec 20, 2013

JK ASAINI HATI YA DHARURA YA MUSWADA WA KUONDOA TOZO YA KODI KWA KADI ZA SIMU.





 
 Rais Jakaya Kikwete ametia saini hati ya dharura (Certificate of Urgency) ili Muswada wa Fedha wa Mwaka 2013 ufanyiwe marekebisho ya kuondoa tozo ya kodi kwa kadi za simu.
 
Bunge la Bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2012/13 lilipitisha kodi ya Sh1,000 kwa kila kadi ya simu, hatua ambayo ilipingwa na wabunge wengi.

Ingawa wasemaji wa Ikulu hawakupatikana jana kuzungumzia suala hilo, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema jana kuwa Rais Kikwete alitia saini hati hiyo juma hili.

Ingawa wasemaji wa Ikulu hawakupatikana jana kuzungumzia suala hilo, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema jana kuwa Rais Kikwete ametia saini hati hiyo juma hili.

“Maana yake ni kuwa, muswada huo unatakiwa urudi bungeni haraka ili uweze kufanyiwa marekebisho hayo,” alisema Makamba. Alisema kabla ya kufikiwa kwa hatua hiyo, Rais alishawaagiza wadau wanaohusika na sekta hiyo wakae na kujadili suala la kodi hizo... “Mazungumzo hayo bado yalikuwa yanaendelea mpaka katikati ya juma hili.”

Hata hivyo, alisema suala la muswada huo kurudishwa bungeni linategemea na ratiba huku akisisitiza kuwa
licha ya Bunge kupitisha muswada huo tangu Julai, mwaka huu, bado kodi hizo zilikuwa hazijaanza kutozwa.

Julai 23, mwaka huu, Rais Kikwete aliagiza mamlaka zinazohusika na kodi na mawasiliano pamoja na kampuni za simu za mikononi, kukutana mara moja kutafuta jinsi gani ya kumaliza mvutano wa kodi hiyo.

Alitoa kauli hiyo alipokutana na viongozi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia na wawakilishi wa kampuni za simu za TTCL, Airtel, Vodacom, Tigo na Zantel, Ikulu, Dar es Salaam.

Alisema lengo kuu la kukutana huko lilikuwa ni kupendekeza jinsi ya kuziba pengo la Sh178 bilioni ambazo zitapotea katika bajeti iwapo kodi hiyo itafutwa.

Wakati wa mvutano wa kodi hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alinukuliwa na vyombo vya habari akisema tozo hiyo haikuwa ya kuwaumiza wananchi, bali mapato yake yalilenga kwenda moja kwa moja kusaidia kueneza umeme vijijini.

0 comments:

Post a Comment