JESHI la Polisi Wilaya ya Nkasi, linamshikilia Pius Jacob, mkazi wa
Kijiji cha Chala kwa kosa la kuoa mwanafunzi wa darasa la tano katika
shule ya msingi Kabwe, wilayani Nkasi.
Mtuhumiwa huyo pia anadaiwa kumuoa dada wa mwanafunzi huyo ambaye ana miaka 16.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Dawati la Jinsia Nkasi, CPL-Anna
Kisimba, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya majirani kutoa
taarifa polisi kuwa mtuhumiwa anaishi kinyumba na wanafunzi hao.
Alibainisha kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya kumchukua kwa
nguvu binti huyo wa darasa la tano mwenye umri miaka 12, na kwenda
kuishi naye kama mke na mume.
“Tulikuwa katika ziara zetu za kawaida zilizoambatana na siku 16 za
kupinga ukatili tukizunguka baadhi ya vijiji vya wilaya yetu, ndipo
raia wema walituarifu kuwepo kwa tukio hilo na kuanza kufuatilia
hatimaye kumkamata mtuhumiwa,” alisema Kisimba.
Aliongeza kuwa mtuhumiwa huyo ameshafikishwa katika Mahakama ya
Wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa Desemba 10 mwaka huu kwa kosa la kumuoa
mwanafunzi na kubaka.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri wa Wilaya ya Nkasi, Oscar
Mdenye, alisema baada ya kufuatilia zaidi waligundua mke wa kwanza wa
mtuhumiwa huyo pia ni mwanafunzi ambaye hata hivyo hakubainisha ni wa
shule gani.
Mdenye, alisema majirani waliwaeleza kuwa mtuhumiwa alimpata mwanafunzi wa pili kwa kutumia nguvu na vitisho.
“Hadi polisi na Ofisi ya Ustawi wa Jamii tunafikiwa na taarifa hizo
inadaiwa mtuhumiwa huyu alikuwa tayari ameishi na binti huyu wa pili
kwa wiki nzima nyumbani kwake, na majirani walijua baada ya binti huyo
kulalamika kwao kuwa alikuwa amechukuliwa kwa nguvu na kulazimishwa
kuolewa,” alisema Mdenye.
Matukio ya ukatili yanayoripotiwa polisi kupitia Dawati la Jinsia na
Watoto Wilaya ya Nkasi yamekuwa yakipungua ambapo mwaka 2012 kulikuwa
na kesi 224 za ukatili zilizoripotiwa ilhali kwa mwaka 2013 ni kesi 143
tu ndizo zilizoripotiwa.
Dec 21, 2013
Afikishwa Mahakamani kwa kuoa wanafunzi wawili ndugu
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment