Nov 28, 2013

Umoja wa Mataifa walaani siasa kimabavu za Israel


Jamii ya kimataifa imeendelea kulaani hatua ya Israel ya kukalia kwa mabavu Quds Tukufu huko palestina. 

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeilaani Israel kwa wingi wa kura kutokana na kukalia kwa mabavu eneo hilo na milima ya Golan ya Syria.

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulikalia kwa mabavu milima ya Golan ya Syria na mashariki mwa Baitul Muqaddas katika kipindi cha vita vya mwaka 1967. Mwaka 1948 Israel pia ilikalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya magharibi mwa mji wa Baitul Muqaddas. 


Umoja wa Mataifa umelaani hatua hiyo ya Israel baada ya mwakilishi wa Syria Bashar al Jaafar kuitaka taasisi hiyo na jamii ya kimataifa kutekeleza majukumu yake mkabala na hatua ya Israel ya kukalia kwa mabavu miinuko ya Golan.

Hii ni katika hali ambayo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jumanne iliyopita liliutangaza mwaka ujao wa 2014 kuwa mwaka wa kuonyesha mshikamano na taifa la Palestina. 

Vilevile Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limezitaka nchi zote wanachama kuitisha matamasha na kufanya shughuli mbalimbali za kuadhimisha mwaka huo. Wakati huo huo nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kushikamana na Wananchi wa Palestina. 

Hafla hiyo ilizohudhuriwa na nchi nyingi wajumbe wa UN na wawakilishi wa taasisi za kimatiafa na zilizo za kiserikali zinazounga mkono mapambano ya taifa la Palestina kwa ajili ya kupata haki zake za msingi. 

Waliohutubia hafla hiyo sambamba na kukaribisha jitihada za kamati maalumu ya kufuatilia haki za taifa la Palestina katika Umoja wa Mataifa, wamesisitiza udharuwa wa Wapalestina kupewa haki zao muhimu kama haki ya kuunda nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa Baitul Muqaddas.

Imeelezwa kuwa, Umoja wa Mataifa umetangaza tarehe 29 Novemba kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya Kutangaza Uungaji Mkono na Taifa la Palestina. 

Kulaaniwa tena sera za mabavu za Israel hasa kitendo cha kulikalia kwa mabavu eneo la Quds na milima ya Golan ya Syria kwa mara nyingine kunaonesha jinsi walimwengu wanavyopinga hatua za Israel za kughusubu ardhi za mataifa mbalimbali. 

Utawala wa Kizayuni wa Israel licha ya kuendelea kukalia kwa mabavu maeneo ya Mashariki ya Kati, siku zote umekuwa ukifanya juhudi za kuhalalisha siasa zake hizo katikaduru za  jamii ya kimataifa. 

Pamoja na hayo kupasishwa kwa mamia ya maazimio na Umoja wa Mataifa yanayolaani hatua hiyo kunabainisha upinzani wa walimwengu dhidi ya sera za kupenda kujitanua za Israel.

Maazimio mengi ya Umoja wa Matafa kuhusiana na mgogoro wa Mashariki ya Kati kama azimio nambari 242 na 338 yanasisitiza ulazima wa kuondoka kikamilifu Israel katika ardhi inazozikalia kwa mabavu za Palestina, Lebanon na Syria. 

Hata hivyo utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukiendelea siasa zake hizo kwa uungaji mkono na madola ya Magharibi hasa Marekani.

Mabadiliko ya kimataifa yanaonesha kuwa, upinzani mkali uliopo hivi sasa dhidi ya Israel umechukua sura mpya na jamii na taasisi za kimataifa kwa njia tofauti, zinapinga sera za kimabavu wa Israel na kuunga mkono haki za wananchi wa Palestina.

Ni wazi kuwa, hatua ya Umoja wa Mataifa ya kulaani sera hizo za Israel ina nafasi muhimu katika kuamsha fikra za waliowengi duniani na kufichua tabia ya kutoheshimu sheria za kimataifa ya utawala huo haramu.

0 comments:

Post a Comment