Mchungaji wa Kanisa la Shakinah Pentecostal la mjini Dodoma, Nabii Elisha
Mliri, ambaye pia ni mume wa marehemu Angela Chibalonza, aliyekuwa
mwimbaji wa nyimbo za Injili, anatuhumiwa kumpa mimba mwanafunzi wa
kidato cha tatu wa Shule ya City High School (jina linahifadhiwa).
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, mama mzazi wa
mwanafunzi huyo, Mary Mkombola (49) alidai kuwa mwanaye alikuwa
akisumbuliwa na mapepo, hivyo akaamua kumpeleka kwa Nabii Elisha ili
aweze kuombewa tatizo hilo lililokuwa likimsumbua.
Mama huyo alisema kuwa mara baada ya kumpeleka binti yake,
alifanyiwa maombi na nabii huyo na kisha kuelezwa kuwa alikuwa
anasumbuliwa na pepo ambalo pia lingemharibia masomo yake.
Kwa mujibu wa mama huyo, baada ya mchungaji kumfanyia maombi binti
yake, alimwambia kuwa atamsaidia kumsomesha kwa kumlipia ada ya mwaka
mzima kutokana na yeye kuwa mjane.
“Alimdanganya atamlipia ada ya mwaka mmoja sh 400,000 ili aendelee
na masomo halafu akaniambia kuwa ataniombea na mimi ili niweze kupata
uwezo wa kuendelea kumsomesha,” alisema mama huyo.
Aliongeza kuwa mara baada ya kukubaliana na mtoto wake, alipeleka
taarifa shuleni ambako aliambiwa apeleke barua ya kuthibitisha kuwa
atakuwa anamlipia ada mwanafunzi huyo.
Mkombola alifafanua kuwa aliongeza kuwa mara baada ya kupeleka barua
shuleni na kukubaliwa, mtoto huyo aliendelea na masomo yake lakini
baadaye alianza kumhisi ni mjamzito.
Alisema kuwa alimuuliza kama ana ujauzito akawa hataki kumwambia
ndipo akaamua kumchapa na kukimbilia kwa mama yake mkubwa maeneo ya
Mbwanga.
“Alipokimbilia kule ndipo akaenda kuwaeleza mama zake wakubwa kuwa
mama ananipiga wakati mimba nimeipata kule alikonipeleka nikafanyiwe
maombi, ikabidi wanipigie simu na kuniambia kuwa mwanangu ana ujauzito
na amepewa na Nabii Elisha.
“Nilimuuliza akanisimulia mambo yote ambayo amekuwa akifanyiwa na
nabii huyo tangu alipopelekwa kufanyiwa maombi mwezi Machi mwaka huu,”
alisema.
Mama huyo aliongeza kuwa waliamua kwenda polisi kutoa taarifa na
kupatiwa fomu ya matibabu kwa ajili ya vipimo ambapo binti huyo
aligundulika kuwa ana ujauzito.
Alisema kuwa walipeleka majibu hayo polisi na kutoa maelezo ambapo
waliambiwa kuwa wasubiri uchunguzi unaendelea na utachukua muda mrefu.
“Tulitoa maelezo polisi mimi na mwanangu na kuambiwa kuwa tusubiri
bado wanafanya uchunguzi lakini muda umepita sasa na mtoto tumbo
linazidi kukua na masomo kasimama bila kujua hatima yake,” alisema.
Alibainisha kuwa mara baada ya baadhi ya viongozi wa kanisa hilo
kupata taarifa, walimfuata mama huyo wakimsihi asilipeleke suala hilo
polisi bali wao watalimaliza.
“Walinifuata watumishi wawili ambao ni Nabii Mgamba na Nabii Monika
wakasema nisifanye lolote wao watamtunza au kama ikiwezekana tuitoe
mimba hii, jambo ambalo sikukubaliana nalo,” alisema.
Naye mwanafunzi huyo alisema kuwa Juni 8, mwaka huu, asubuhi
alipigiwa simu na Nabii Elisha akamwambia aende mjini na alipofika
alimpakia kwenye gari lake na kwenda naye kwenye nyumba ya kulala wageni
iliyoko maeneo ya jirani na Chuo cha CBE mjini hapa.
“Nilimuuliza tunakwenda wapi, akaniambia tunakwenda kanisani lakini
cha kushangaza tulilipita kanisa, hivyo nikawa na wasiwasi lakini kabla
hatujafika tulikokuwa tunakwenda tukapita sehemu akaongeza upepo
kwenye tairi,” alisema.
Kwamba baada ya kujaza upepo, waliondoka na kwenda katika nyumba
hiyo ya kulala wageni lakini kabla hawajashuka alimpatia soda aina ya
Fanta akanywa na muda mfupi akapoteza fahamu kidogo na alipozinduka
akajikuta anafanya mapenzi na mchungaji huyo.
“Nilijikuta kifuani mwa nabii tukiwa wote watupu, nikaanza kulia,
akanibembeleza na kuniambia ‘unafikiri kukulipia ada yote hiyo ilikuwa
ni bure’ mbona wapo watu wengi sijawalipia ada, lazima nifanye na wewe
mapenzi mara tano, kwa hiyo bado mara nne nitafanya na wewe hata kwa
nguvu na ukimwambia mtu nitakuua kwa maombi,” alisema.
Binti huyo alidai kuwa tangu siku hiyo hakuweza kuziona siku zake
tena mpaka mama yake alipoanza kumhisi kuwa ana ujauzito na kumpeleka
kupima na kubainika ni kweli.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Suzan Kaganda, alithibitisha
kuwa tayari walikwisha kuyapokea malalamiko ya mwanafunzi huyo na
wanayafanyia kazi.
“Tunayafanyia kazi, kwani tulipata malalamiko hayo lakini tunasubiri
hadi atakapo jifungua tuweze kutumia kipimo cha vinasaba (DNA)
kuthibitisha aliyempa ujauzito,” alisema.
Alipotafutwa Nabii Elisha alisema kuwa hayuko Dodoma kwa wakati huu na kumtaka mwandishi aende polisi atapata maelezo zaidi.
Nov 14, 2013
POLISI Yadaiwa Kumlinda Mchungaji Mbakaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment