WATUHUMIWA 11 waliokamatwa wakifanya mafunzo ya kijeshi yenye asili
ya kigaidi msituni katika Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara wameongezeka
na kufikia 13, ambapo kesi yao itaendelea leo katika Mahakama ya Wilaya
Nanyumbu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara,
Zelothe Stephen alisema wamekamata watu wengine wawili na kufikia idadi
ya watu 13 na kwamba uchunguzi unaendelea kwani kuna mambo mengi
yanahitaji uchunguzi wa kina.
Kamanda Stephen alisema watuhumiwa wa awali walikuwa wamefikishwa
katika Mahakama ya Wilaya ya Nanyumbu na sasa wanafanya utaratibu ili
kesi yao iweze kuhamishiwa Mahakama ya Mkoa wa Mtwara.
“Idadi ya watu waliokamatwa wakifanya mazoezi yenye asili ya kigaidi
katika Wilaya ya Nanyumbu kutokana na vifaa walivyokuwa wakitumia sasa
imeongezeka na kufikia 13, baada ya kuwakamata wengine wawili,” alisema
Stephen.
Kamanda aliongeza kuwa, walitegemea kesi ya watuhumiwa hao
ingehamishiwa mahakama ya mkoa, lakini bado kuna taratibu za kisheria
ambazo ni lazima zifuatwe na kwamba, wanasheria wapo kwenye mchakato
kuona sheria zinazotumika zinatazamwa kwa kina kuona ni nini mashtaka
yao.
“Tulitegemea kesi yao ingehamia hapa, lakini kuna mambo ya kisheria
ambayo ni lazima yafuatwe, hivyo tukitoka hapa tunakwenda kumalizia
taratibu ili wahamie huku, haya ni mambo ambayo hayaishi kienyeji,”
alisema.
Kamanda Stephen alisema vijana hao wanatuhumiwa kwa tuhuma za kupata mafunzo ya kijeshi msituni kwa kutumia CD za Al-Shabaab.
“CD hizo zilikuwa zinatoa mafunzo ya kigaidi ya kundi la Al-Shabaab
ya kuchinja watu, mauaji ya Osama Bin Laden, Zindukeni Zanzibar, kuandaa
majeshi, mauaji ya Idd Amin na Mogadishu Sniper,” alisema.
Alisema
watuhumiwa wote ni wakazi wa Wilaya ya Nanyumbu mkoani hapa na kwamba,
walikuwa wakiongozwa na Mohamed Makande (39), mkazi wa Kijiji cha
Sengenya ambaye pia anashikiliwa na jeshi hilo.
Aliwataja wengine waliokamatwa kuwa ni Hassan Omary (39) mkazi wa
Kijiji cha Nanyulu, Rashid Ismail (27), Abdallah Hamisi (32), Salum Wadi
(38), Fadhili Rajabu (20), Abbas Muhidini (32), Ismail Chande (18),
Said Mawazo, Issa Abeid (21), na Ramadhani Issa (26) wote wakazi wa
Kijiji cha Likokona.
Oct 18, 2013
Watuhumiwa wa Mafunzo ya Kijeshi waongezeka
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment