WANANCHI wa kijiji cha Murugwanza, wilayani Ngara, mkoani Kagera, wamelituhumu jeshi la polisi wilayani humo kuwa baadhi ya askari wamekuwa na tabia ya kutoa siri wanazopewa na raia kuhusu matukio mbalimbali ya uhalifu na kusababisha dhana ya polisi jamii kutoweka.
Wananchi hao walitoa tuhuma hizo dhidi ya jeshi la polisi kwenye mkutano wa uzinduzi wa dhana ya elimu ya polisi jamii katika tarafa ya Nyamiaga uliofanyika katika kijiji cha Murgwanza katika mamlaka ya mji mdogo wa Ngara.
Mkutano huo ulioitishwa na maafisa wa jeshi la polisi kitengo cha polisi jamii kutoka ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi wilayani Ngara (OCD), ili kutoa elimu ya ulinzi shirikishi katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa kijiji hicho, Edwin Bitwale, alisema kitendo cha baadhi ya polisi kupewa taarifa kuhusiana na wahalifu na ndani ya muda mfupi taarifa hizo husambaa mitaani, hali ambayo inakatisha tamaa wananchi na kukosa imani kwa jeshi hilo.
“Tuna hofu kwamba maisha yetu yako hatarini kwani mhalifu aliyetajwa anaanza kumtafuta aliyetoa taarifa hizo polisi na anaweza kuunda kikosi cha kummalizia mtoa siri,” alisema Bitwale.
Alisema polisi hawawajibiki kulinda na kutetea viapo wanavyoapa katika mafunzo na kusababisha taifa kuwa na askari wasio wazalendo.
Aliongeza kuwa katika kuvujisha siri askari hao wanapewa hongo ili wawalinde wahamiaji haramu ambao wanaendelea kuishi nchini kinyume cha sheria kwenye harakati za utekelezaji wa Operesheni Kimbunga, awamu ya pili.
Kwa upande wake afisa polisi jamii tarafa ya Nyamiaga Respicius John alisema ni kosa la jinai kwa askari polisi kutoa siri za mteja na kwamba kufanya hivyo ni kuvunja kiapo katika utumishi wake.
John aliwataka wananchi kutoa taarifa mara moja kwa viongozi wa ngazi za juu wa jeshi hilo ili polisi mvujisha siri aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
0 comments:
Post a Comment