Aug 27, 2013

MZEE WA MIAKA 80 AJINYONGA MOROGORO



WATU wanne wamefariki dunia mkoani Morogoro katika matukio tofauti, likiwamo la mzee wa miaka 80 kujinyonga kwa kamba ya ukindu baada ya kutengwa na watoto wake na kumsababishia ugumu wa maisha. Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alimtaja mzee huyo kuwa ni Philipo Ernest (80) wa Kijiji cha Vidunda Tarafa ya Mikumi wilayani Kilosa.
Alisema alijinyonga Agosti 24 asubuhi kwenye mti nyuma ya nyumba yake.

Shilogile alisema pia kuwa mwenda kwa miguu, Abuu Juma (7) mkazi wa Mkundi Manispaa ya Morogoro alifariki dunia papo hapo kwa kugongwa na basi la Kampuni ya Zenji bar linalofanya safari zake kati ya Turiani Wilaya ya Mvomero na Morogoro mjini.

Alisema ajali hiyo ilitokea Agosti 25 jioni katika eneo la Mandela Tankini Kata ya Magole wilayani Kilosa.

Basi hilo dogo la Nissan lilikuwa likiendeshwa na Devis Pius (29) ambaye anashikiliwa na polisi.

Kamanda alisema tukio la tatu lilitokea Agosti 24 asubuhi katika shamba la mkonge Kingolwira Manispaa ya Morogoro.

Alisema msimamizi wa shamba hilo aligundua mwili wa maiti ya kike ndani ya shamba hilo, ambayo hadi sasa haijafahamika jina.

Mwili huo baada ya kufanyiwa uchunguzi ilionekana mtu huyo alinyongwa na kichwa chake kupasuliwa na kitu kizito. Hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo.

Kamanda Shilogile alisema mwanamke Kabura Matiga (53) alikutwa amejinyonga kwa kanga chumbani kwake katika Kijiji cha Kiberenge, Ludema wilayani Kilosa..

Chanzo cha kujinyonga hakijafahamika na polisi wanaendelea na uchunguzi, alisema.