Aug 26, 2013

Mapigano yazuka tena Goma Mashariki mwa Congo


Mapigano mapya yamezuka mwishoni mwa juma katika eneo la Goma, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo ripoti zinasema watu watatu walifariki baada ya makombora kurushwa katika maeneo ya makaazi ya watu.
Haijulikani ni nani aliyerusha makombora hayo lakini wanainchi wameandamana wakililaumu jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa MONUSCO kwa kile wanachodai limewashambulia waasi katika juhudi za kuwatimua kwenye eneo hilo.
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wamewalaumu waasi kwa kurusha makombora hayo lakini hakuna kundi lolote la waasi ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo.
Afrika Kusini, ambayo imechangia kikosi hicho cha kulinda amani, imekiri kuwa mwanajeshi wake mmoja amejeruhiwa katika mlipuko huo wa bomu.
Akizungumza kwa simu na BBC, Msemaji wa jeshi la Afrika Kusini, Brigedia Generali Kolani Mabanga, amesema mwanajeshi wake mmoja alijeruhiwa vibaya na kwa sasa anaendelea kupata matibabu huku mipango ya kumrejesha nyumbani kwa matibabu zaidi ikiendelea.
Hali ya ulinzi imeimarisha katika eneo hilo lakini wakaazi wa mji huo na viunga vyake wanasema hali bado ni ya wasi wasi.