Aug 16, 2014

“Palestina ndio kadhia kubwa zaidi kwa Waislamu”

Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kukaliwa kwa mabavu Palestina ndio kadhia kubwa kabisa katika ulimwengu wa Kiislamu. 

Dakta Ali Larijani amesema hayo leo katika ujumbe wake kwa Kongamano la Muungano wa Jumuiya za Kiislamu za Wanachuo wa Ulimwengu wa Kiislamu ambapo sambamba na kutoa mkono wa pongezi kwa mnasaba wa kumbukumbu ya ushindi wa muqawama wa Kiislamu wa Lebanon dhidi ya utawala haramu wa Israel katika vita vya siku 33, ametoa wito wa kuzingatiwa zaidi kadhia ya Palestina.

Spika wa Bunge la Iran amesema kuwa, ili kukabiliana na adui wa pamoja kuna haja ya kuweko ushirikiano wa kila upande wa Waislamu sambamba na kulinda umoja na mshikamano baina yao. 

Spika Larijani ameeleza kusikitishwa kwake na jinsi ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa ulivyokumbwa na makundi mabaya ya kufurutu ada ambayo yamekuwa yakikuza hitilafu ndogo zilizoko baina ya Waislamu na hivyo kufanya njama za kuvuruga umoja miongoni mwa Waislamu.

0 comments:

Post a Comment