Aug 14, 2014

Mashambulio ya waasi wa LRA yapamba moto CAR


Mashambulio ya wanamgambo wa kundi la waasi wa LRA la nchini Uganda yanazidi kupamba moto siku hadi siku huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Taarifa zinasema kuwa, kundi la waasi wa LRA la nchini Uganda kwa miaka kadhaa limekuwa likitekeleza mashambulio na kufanya mauaji huko kaskazini mwa Uganda, Sudan Kusini, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na hivi sasa limejizatiti katika eneo la kusini mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Kiongozi mmoja wa Asasi ya Kiraia katika Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema kuwa, kila wiki wanamgambo wa LRA wanavishambulia vijiji, wanafanya mauaji, ubakaji, uporaji na kuwateka nyara wenyeji wa eneo hilo. 

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa, kundi la LRA limeshauwa zaidi ya watu laki moja katika eneo la katikati mwa Afrika katika kipindi cha miaka 27 iliyopita. 

Kundi hilo pia linatuhumiwa kuwateka nyara zaidi ya watoto elfu sitini. 

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC inamsaka Joseph Kony kiongozi wa LRA na baadhi ya wasaidizi wake kwa kutenda jinai za kivita na zilizo dhidi ya binadamu.

0 comments:

Post a Comment