Aug 17, 2014

Mahakama: Mansour ana haki ya dhamana


Aliyekuwa Mwakilishi wa Kiembe Samaki, Mansour Yusuf Himid
Aliyekuwa Mwakilishi wa Kiembe Samaki, Mansour Yusuf Himid


MAHAKAMA Kuu ya Zanzibar, imesema haina pingamizi na ombi la dhamana kwa aliyekuwa Mwakilishi wa Kiembesamaki, Mansour Himid Yussuf.

Imesema kutokana na ombi hilo, mahakama imebaini kuwa limezingatia vigezo vyote vya kisheria.

Ombi hilo la dhamana liliamuliwa jana  baada ya mawakili wa upande wa utetezi na Serikali kuvutana kisheria mahakamani hapo.

Baada ya mabishano hayo ya kisheria, anayesikiliza ombi hilo, Jaji Abraham Mwampashi, alisema pamoja na kuwasilishwa kwa hoja, mtuhumiwa ana haki ila aliomba apewe muda ili aweze kupitia shauri hilo na kutoa uamuzi Agosti 18, mwaka huu.

“Hoja zote nimezisikiliza kwa umakini, hivyo naomba nipewe muda hadi Agosti 18, ambapo kesi ya msingi itasikilizwa hivyo hoja hizo nitazitolea uamuzi,” alisema Jaji Mwampashi.

Alisema kuwa endapo atapewa muda wa kutosha atapitia hoja hizo kwa pande zote mbili na kutoa uamuzi wa kumpatia, au kutompatia mtuhumiwa huyo dhamana kwa mujibu wa sheria ya Zanzibar.

Mapema jopo la mawakili wanaomtetea Mansour kutoka Kampuni ya Imma Advocates, wakiongozwa na Gasper Nyika, walisema kwa mujibu wa kifungu cha 150 (4) cha sheria ya mwaka 2004 sheria ya Zanzibar, hakuna kosa lolote ambalo linaweza kumyima mtu dhamana endapo shauri hilo litapelekwa katika ngazi ya Mahakama Kuu, kwani ina uwezo wa kutengua uamuzi wowote.

Hoja nyingine ni kuwa mtuhumiwa huyo ni mkazi wa Zanzibar anayeishi na familia yake katika maeneo ya Chukwani, Unguja, hivyo hawezi kukimbia endapo akipewa dhamana hiyo.

“Mheshimiwa Jaji tunaiomba mahakama yako tukufu itoe uamuzi utakaokuwa umetenda haki ya pande zote mbili, lakini ikizingatiwa mteja wetu kwa muda aliokaa rumande anaweza kuathirika kisaikolojia, pia akipewa dhamana apate kuungana na familia yake huku kesi ya msingi itakuwa inaendelea,” alisema Wakili Gaspar.

Upande wa wapingaji wa dhamana hiyo, ukiongozwa na Raya Mselem kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ulipinga maombi hayo, huku ukidai kuwa mtuhumiwa Mansour nyaraka zake za umiliki wa silaha zina kasoro.

Mselem alisema kifungu cha 150(1) kinaeleza makosa ya jinai ikiwamo usafirishaji wa dawa za kulevya, mauaji ya makusudi, wizi wa kutumia silaha, uhaini, pamoja kumiliki silaha kinyume na sheria na hayana dhamana.

Alisema wana shaka na umiliki wa silaha yake kwani alipewa na kusainiwa upande wa Tanzania Bara, akiwa ni mkazi wa Upanga jijini Dar es Salaam hali ya kuwa makazi yake ni Chukwani, Zanzibar.

Agosti 2, mwaka huu, Jeshi la Polisi Zanzibar lilimtia mbaroni Mansour, baada ya kufanya upekuzi katika nyumba yake na kufanikiwa kukamata silaha aina ya shotgun yenye namba za usajili 1904136413 aina ya Bore Browning pamoja na risasi 112.

Silaha nyingine aliyokamatwa nayo ni bastola yenye namba F76172W pamoja na risasi 295, jambo ambalo ni kinyume na sheria ya umiliki wa silaha za moto, ambapo mmiliki anatakiwa kuwa na risasi zisizozidi 25.

0 comments:

Post a Comment