Aug 17, 2014

JIWE LAVUNJA NYUMBA NA KUUA

Mvua yaua sita Mwanza, Kagera


Baadhi ya wakazi wa Mwanza wakiangalia nyumba iliyoporomokewa na mwamba katika Mtaa wa Nyerere A Sinai-Mabatini jana.
Baadhi ya wakazi wa Mwanza wakiangalia nyumba iliyoporomokewa na mwamba katika Mtaa wa Nyerere A Sinai-Mabatini jana.
WATU sita wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa katika matukio mawili tofauti yaliyoambatana na mvua katika mikoa ya Mwanza na Kagera.

Katika tukio la jijini Mwanza, vilio na simanzi jana vilitawala kwa wakazi wa maeneo ya Sinai-Mabatini, baada ya vifo vya watu wanne wa familia mbili tofauti, vilivyotokana na mvua iliyosababisha miamba mikubwa ya mawe kuporomoka na kuponda nyumba zao usiku wa manane.

Tukio hilo la kusikitisha limeripotiwa kutokea saa nane usiku kuamkia jana, wakati mvua iliyoambatana na upepo wa wastani ilipokuwa ikiendelea kunyesha, na kusababisha miamba hiyo mikubwa inayokadiriwa kufikia tani mbili kuporomoka na kuziponda nyumba hizo na kusababisha vifo hivyo na majeruhi wanne.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari wakati wa mvua.

Nyumba zilizokumbwa na maafa hayo zinamilikiwa na watu waliotajwa kwa majina ya Joseph William na Lameck Ajiji, na kila moja watu wawili wamefariki kwa kukandamizwa na miamba hiyo.

Katika nyumba ya William iliyokuwa na watu watano, waliofariki wametajwa kuwa ni Kefa Joseph (15) na Emmanuel Joseph (12), wote mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbugani na majeruhi mmoja ambaye hakufahamika jina lake ambaye alikimbizwa hospitali.

Nyumba inayomilikiwa na Ajiji yenye watu watatu, waliofariki wametambuliwa kuwa ni mama wa nyumba hiyo, Kwinta Geko (24) na mumewe Samson Odinya.

Waliojeruhiwa ni mtoto Bety Samson (4) na Godfrey Joseph (14) mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbugani.

Tukio hilo ni la pili kutokea katika eneo hilo la Sinai. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2009 baada ya miamba kuporomoka na kusababisha vifo vya watu wawili wa familia moja.

Tukio la jana lilivuta hisia tofauti kwa wakazi wa Jiji la Mwanza, huku wengine wakiangua vilio.

0 comments:

Post a Comment