Aug 16, 2014

Jaji azuia Dhamana ya mansour Mansour


Ni Mansour Yussuf Himid akiwa kwenye chumba maalumu cha kuskiliziwa kesi hapo Mahakama kuu Vuga. Shemeji ya Rais mstaafu, Amani Karume, Mansour Yussuf Himid (pichani), anaendelea kusota rumande kutokana na ombi lake la dhamana lililofikishwa Mahakama Kuu Zanzibar kutotolewa uamuzi.

Wakiwasilisha ombi hilo la dhamana mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Vuga, Abraham Mwampashe, mawakili wa Mansour wakiongozwa na Gaspa Nyika, walisema Mahakama Kuu ina haki ya kumpa mtu dhamana chini ya kifungu cha 150 cha sheria ya mwaka ya Zanzibar.

Alisema kwa kuwa mtuhumiwa ni raia wa Tanzania na hana rekodi ya uhalifu na hajawahi kutiwa hatiani kwa kosa la jinai, hivyo mahakama kuangalia misingi ya kumpa dhamana.

Ombi hilo la Mansour kutaka kupatiwa dhamana linatokana na kushtakiwa kwa makosa matatu, la kwanza likiwa kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Raya Mselem, ni kumiliki silaha, kinyume cha sheria.

Raya akisaidiwa na Maulid Ali litaja tuhuma nyingine zinazomkabili Mansoor kuwa ni kupatikana na risasi 295 kinyume cha kifungu cha 6 (3) na 34 (1) (2) sheria namba 7 ya Zanzibar ya mwaka 1964, na kosa la tatu ni kupatikana na marisau (risasi za shotgun) 112 kinyume cha kifungu cha 34 (1)(2) sheria ya risasi na silaha namba 2 ya mwaka 1991. 

Akiwa mahakamani hapo, Raya aliendelea kupinga ombi la dhamana la mshtakiwa huyo kutokana na tuhuma ya kwanza dhidi ya Mansour ya kumiliki risasi nyingi kinyume cha sheria ya Zanzibar kwamba, halina dhamana
Alidai mshtakiwa huyo ameidanganya mahakama, kwani leseni ya umiliki wa silaha aliyonayo ni ya mwaka 2010 ya Tanzania Bara na inaeleza kuwa anaishi Upanga, jijini Dar es Salaam. 

“Kama leseni yake inavyojieleza kuwa anaishi Upanga, hivyo amekiuka kanuni na sheria za Zanzibar, kwani mshtakiwa huyo angepaswa silaha hizo kuwa nazo Upanga Dar es Salaam na siyo Chukwani, Zanzibar alikokamatwa nazo,” alidai Raya.

Aliitaka mahakama hiyo kuzingatia sheria na kanuni, hivyo mtuhumiwa huyo kutopatiwa dhamana kwa mujibu wa tuhuma zinazomkabili.

Alisisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kutokiuka sheria bila ya kujali cheo, utajiri au jinsia, kwani kila mmoja yupo sawa katika kutii sheria za nchi. 

Jaji Abraham Mwampashe alishindwa kutoa dhamana na kuamuru mtuhumiwa huyo kurejeshwa rumande hadi Agosti 18, mwaka huu, kesi yake itakaposikilizwa tena.

0 comments:

Post a Comment