Apr 25, 2014

UWANJA WA MAARIFA;Hadi Lini Utakuwa Mwenye Kughafilika?

 
Anasema Allaah  سبحانه وتعالى
 
 
(وَلَقَدْ ذَرَأْنَا لِجَهَنَّمَ كَثِيرًا مِّنَ الْجِنِّ وَالإِنسِ لَهُمْ قُلُوبٌ لاَّ يَفْقَهُونَ بِهَا وَلَهُمْ أَعْيُنٌ لاَّ يُبْصِرُونَ بِهَا وَلَهُمْ آذَانٌ لاَّ يَسْمَعُونَ بِهَا أُوْلَئِكَ كَالأَنْعَامِ بَلْ هُمْ أَضَلُّ أُوْلَئِكَ هُمُ الْغَافِلُونَ)   
(Na kwa yakini Tumeiumbia [moto wa] Jahannamu majini wengi na watu. Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. 
 Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama, bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walioghafilika) [Al-A'araaf: 179]
Ni ahadi ya kutisha kwa walioghafilika na Allaah na wasio na khofu kuhusu adhabu ya moto Siku ya Qiyaamah.  
Wale ambao wamepambika katika matamanio na starehe za dunia na ambao wameathirika nayo na wakaiuza Akhera yao kwa dunia. Watu wasiomkumbuka Mola wao ila kidogo tu. 

Allaah سبحانه وتعالى Ametaja hapa, kuwa Jahannam itajaa watu na majini ambao Amewafananisha kama wanyama, bali Amewaona kuwa wao ni wapotofu zaidi kuliko wanyama kwani wanyama angalau wanajua yepi ya kuwafaa na yepi  ya kuwadhuru kisha hujiepusha nayo.

Ee ndugu Muislamu unayelala huku Swalaah za fardhi zikakupita au ukazichelewesha Swalaah zako bila ya sababu, mpaka lini utakuwa katika kughafilika?  Haukushituka moyo wako kwa kitisho kama hiki cha maneno ya Allaah سبحانه وتعالى  

(فَوَيْلٌ لِّلْمُصَلِّين)  ( الَّذِينَ هُمْ عَن صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ )
(Basi, ole wao wanaoswali)  (Ambao wanapuuza Swalaah zao) [Al-Maa'uun :4-5
Ee ndugu Muislamu uliyeuweka moyo wako ukawa mbali na dhikru-Allaah ukaihama Qur-aan, mpaka lini utakuwa katika kughafilika?

Ndugu Muislamu uliyetega sikio lako kwa kusikiliza nyimbo na maneno ya umbea, mpaka lini utakuwa katika kughafilika? 

Ndugu Muislamu unayetazama mambo yaliyoharamishwa mpaka lini utakuwa katika kughafilika?

Ndugu Muislamu unayeyasoma haya na ukatambua mabaya yako na tukatambua sisi mabaya yetu, tujiulize sote  mpaka lini tutakuwa katika kughafilika? 

Tuamke na kujikurubisha kwa Allaah ili kuepukana na maradhi haya ya kughafilika kabla haijafika siku ya majuto, siku ambayo kila mtu atatamani irudi nyuma ili apate kujirekebisha lakini haitowezekana!

0 comments:

Post a Comment