Feb 21, 2014

Tanzania kupeleka majeshi Sudan Kusini


 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, 

Dar es Salaam jana.Serikali inatarajia kupeleka kikosi kimoja cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Sudan Kusini kwa ajili ya kulinda amani kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema Dar es Salaam jana kwamba Serikali imekubali kupeleka batalioni moja baada ya kuombwa na Umoja wa Mataifa (UN).
Sudan ya Kusini imekuwa katika machafuko ambayo yamesababisha vifo vya mamia ya raia na wengine kujeruhiwa.
 “Tumefanya uamuzi wa kupeleka majeshi yetu Sudan Kusini, tumefanya hivyo baada ya kuombwa na Umoja wa Mataifa kwa sababu ya ubora wa jeshi letu,” Membe aliwaambia waandishi wa habari.
Alisema jukumu la kulinda amani katika Bara la Afrika ni la Waafrika wenyewe na kwamba Tanzania inajiona kwamba ina jukumu la kusaidia kupatikana kwa amani.
Alisema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon alimwomba Rais Jakaya Kikwete kusaidia kupeleka majeshi yake Sudan Kusini kusaidia kulinda amani.

 “Rais alikubali, sasa tuko kwenye maandalizi, nadhani Aprili jeshi letu litaondoka kuelekea Sudan Kusini,” alisema Membe.
Kwa sasa Tanzania ina vikosi vya wanajeshi wa kulinda amani katika nchi za DRC, Darfur (Sudan) na Lebanon.
Mgogoro Ziwa Nyasa
Kuhusu mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa, Membe alisema utapatiwa ufumbuzi mwezi ujao baada ya mawaziri na maofisa wa nchi hizo kuwekwa kitimoto na Kamati ya Rais Joaquim Chisano wa Msumbiji na viongozi wengine wastaafu.
Membe alisema wanaotakiwa kwenda kuhojiwa ni yeye na maofisa wake na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema…

 “Baada ya pande mbili za viongozi kutoka Tanzania na Malawi kuwekwa kitimoto, ndipo uamuzi utatolewa.”
Alisema anaamini kwamba uamuzi huo utakuwa mpaka kuwa katikati ya Ziwa Nyasa, badala ya ziwa lote kuwa mali ya Malawi.
Alisema kama uamuzi utakuwa ziwa lote kuwa mali ya Malawi, Tanzania itawasilisha mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro (ICJ).

0 comments:

Post a Comment