WACHINA wawili wa Kiwanda cha Urafiki Plastic cha jijini Dar es Salaam wanashikiliwa na polisi wa Kituo cha Magomeni kwa tuhuma za kukutwa na kiganja cha mfanyakazi wao, Jumanne Rashid, kilichofukiwa kwenye eneo la kiwanda hicho.
Akielezea tukio hilo kwa waandishi wa habari jana, ndugu wa Jumanne aliyejitambulisha kwa jina la Rehema Rashid, alisema Novemba 17 mwaka huu majira ya saa 3:00 usiku walipata taarifa kuwa ndugu yake alipata ajali ya kukatwa mkono na mashine kiwandani hapo.
Alisema baada kupata ajali hiyo, Wachina hao kwa kusaidiana na wafanyakazi wengine walimpeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu, ambapo ndugu wote waliendelea na huduma ya kumuuguza.
Rehema alisema jana wakiwa katika pilikapilika za kwenda kumjulia hali ndugu yao, walipata taarifa kwa wasamaria wema kwamba kiganja cha mkono wa ndugu yao kimeonekana kikiwa kimefukiwa pembezoni mwa kiwanda hicho.
“Leo asubuhi tukiwa katika maandalizi ya kwenda kumwona Jumanne, tulipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema ambao wanafanya shughuli za kufua vyuma chakavu karibu na kiwanda hicho wakitutaka twende kutambua kama kiganja kilichofukiwa ni chake,” alisema Rehema.
Rehema alisema akiwa na ndugu zake walielekea kiwandani hapo na mmoja wa ndugu zake, Allo Said, alipokiangalia kiganja hicho alibaini kuwa ni cha ndugu yake, Jumanne Rashid.
Alisema baada ya kuona kiganja hicho, walishikwa butwaa, kwa kuwa walielezwa na Wachina hao kuwa baada ya Jumanne kukatwa na mashine mkono wote kuanzia eneo la begani ulisagika na hakuna kilichobakia.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) wa Kinondoni, Camillius Wambura, alikiri kwamba Wachina hao, Yu Xiawey na Li Shlin wanashikiliwa kwa mahojiano katika Kituo cha Polisi Magomeni kuhusiana na tukio hilo.
RPC alisema taarifa walizonazo hadi sasa ni kwamba Jumanne alipatwa na mkasa huo usiku wa Jumapili iliyopita baada ya kutakiwa kusafisha mashine iliyokuwa imezima ghafla.
Alisema polisi inachunguza kubaini endapo ajali hiyo ilikuwa ya kupanga au bahati mbaya.
0 comments:
Post a Comment