Nov 15, 2013

Polisi Kukiadabisha Chombo Cha Habari

JESHI la Polisi Kikosi cha Wanamaji Bandarini Tanzania  limesema litakichukulia hatua za kisheria chombo cha habari kilichoripoti habari kuhusu wizi wa kontena la kompyuta za Rais, Paul Kagame wa Rwanda.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi ambaye ni Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji Bandari, Mboje Kanga alisema jeshi hilo limesikitishwa na habari iliyotolewa na chombo hicho kuwa watuhumiwa wa tukio hilo hawajakamatwa.

Alisema taarifa za chombo hicho zinadai kuwa jalada hilo limekaliwa na watuhumiwa hawajakamatwa, jambo ambalo si kweli watuhumiwa wanne wamekamatwa na kesi hiyo ipo katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke na kusajiliwa kwa namba 499/2012 na ipo katika hatua ya usikilizwaji na itasilikizwa tena, Novemba 18 mwaka huu.

Hata hivyo, alisema chombo hicho kilidai kuna madini ya shaba yaliyokuwa yanasafirishwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda nchini Zambia yaliibiwa, ambapo ukweli ni kwamba madini hayo yalikuwa yanatokea Zambia na yalikuwa katika bandari hiyo ili yasafirishwe kwenda ng’ambo.

Pia alisema uchunguzi ulifanyika na watuhumiwa wanane walikamatwa na kesi iko Mahakama ya Wilaya ya Temeke na  kusajiliwa namba 752/2012 na ipo katika hatua ya usikilizwaji, ambapo itasikilizwa, Novemba 19 mwaka huu.

Alisema tukio la wizi wa mafuta bandarini ni la kweli na liliripotiwa kituo cha Polisi Kilwa Road, uchunguzi ulifanyika na watuhumiwa wanne walikamatwa na kufikishwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Temeke na kusajiliwa kwa namba 747/2012 na ipo katika hatua ya usikilizwaji.

0 comments:

Post a Comment