Nov 27, 2013

OIC yalaani kupigwa marufuku Uislamu Angola



Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imelaani na kukosoa vikali uamuzi wa serikali ya Angola wa kuipiga marufuku dini ya Kiislamu nchini humo. 

OIC imetoa taarifa na kusema imesikitishwa na kushangazwa na uamuzi wa serikali ya Angola wa kuipiga marufuku dini ya Kiislamu na kuzitaka jumuiya na taasisi zote duniani kulaani vikali hatua hiyo. 
Taarifa ya OIC pia imeutaka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, nchi zinazozungumza lugha ya Kireno na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) kuchukua msimamo madhubuti wa kukabiliana na uamuzi huo wa serikali ya Angola. 

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imesema uamuzi wa Angola wa kuipiga marufuku dini ya Kiislamu unakiuka sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu na uhuru wa kuabudu. 

Wizara ya Utamaduni ya Angola imetangaza kuwa dini ya Kiislamu ni marufuku nchini humo na kwamba sasa serikali hiyo imeamua kuibomoa misikiti yote nchini humo. 

Serikali ya Angola imedai kuwa Uislamu si dini bali ni tapo tu la imani.

Wakati huohuo mtandao wa habari wa Al Misril Yaum umemnukuu Mkuu wa masuala ya habari wa chama tawala nchini Angola MPLA akisema kuwa hakuna msikiti wowote utakaofungwa nchini humo. 

Ramadhan Shiblolo amesema Uislamu ni moja ya dini muhimu zaidi duniani na kwamba habari za kufungwa misikiti nchini Angola hazina ukweli. 

Huku akiashiria kuwepo misikiti mia moja nchini humo amesema Angola katu haitoupiga marufuku Uislamu. 

Katika upande mwengine Sheikh Othman bin Zaid, Imamu wa msikiti wa Nurul Islam ulioko katika mji mkuu wa Angola Luanda amesema serikali haijachukua uamuzi wa kufunga misikiti na kwamba mkuu wa masuala ya kiutamaduni na kidini wa serikali amekanusha habari za kuchukuliwa uamuzi kama huo. 

Sheikh Zaid amesema kuna misikiti miwili iliyobomolewa kutokana na kujengwa katika eneo ambalo halikuwa limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa misikiti.

0 comments:

Post a Comment