Oct 4, 2013

Mzee Mwinyi Awaaga Mahujjaji


 VIONGOZI WA TANZANIA MUSLIM HAJJ TRUST WAKIOMPOKEA MZEE MWINYI

Rais mstaafu awamu ya pili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Al haj Ally Hassan Mwinyi,amewaaga Mahujaji.

Hafla hiyo fupi iliyoandaliwa na Tanzania Muslim Hajj Trust imefanyika hivi punde katika ukumbi wa Starlight Hotel uliopo jijini Dar es salaam.

Akitoa nasaha zake kwa waumini waliohudhuria maagano hayo,mzee mwinyi alisema ibada ya hija ni ibada inayoambatana na bahati kutoka kwa Mwenyezi Mungu,hivyo unavyoipata nafasi hiyo unatakiwa uitumie kwa ufanisi zaidi.

"Ndugu zangu mahujaji,nawapeni hongera,lakini kuhiji ni bahati,ndiyo maana wengi wetu tunahiji tukiwa ni wazee,bila shaka katika ujana wetu tulikuwa tuna nia ya kwenda kuhiji lakini,hatukujaaliwa,na sasa bahati imetuangukia,basi tuitumie vizuri"Alisema.

Aliendelea kusema kwamba,"Tunachotaraji baada ya kurudi kwenu ni kuondokewa na madhambi,sasa ukitaka kuyarudisha hayo madhambi kidogo kidogo hiyo ni shauri yako",mwisho wa kumnukuu.

Awali akiongea katika hafla hiyo,katibu mkuu wa Tanzania Muslim Hajj Trust  Al haj Abdallah Jabir aliwatahadharisha mahujaji muda wote wa safari kuwa makini na ukarimu watakaopewa na watu wasiowajuwa.

"Tumepokea barua kutoka Serikali ya Saud Arabia kwamba kuna baadhi ya watu wa Asia,wanawakarimu  mahujaji kwa vinywaji  vikiwa vina madawa ya kulevya na baada ya kupatwa na usingizi wanawaibia kila kitu",alisema.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa manispaa ya Mtwara Mikindani Sheikh Suleyman Ahmad Mtalika alisema,"Hadi sasa sijaamini kama nami ni mmoja wa mahujaji,kwani ni azma ambayo nilikuwa nayo muda mrefu sana,namuomba Mungu anipe afya njema ili nikaifanye Ibada ya Hijja kikamilifu hatimaye nikirudi nitoe muongozo mwema kwa familia yangu".

Naye Ustaadh Abdu Shakuor Maulid wa Madrasat Qadiriyyah kutoka Dodoma mjini,akiongea na Munira blog amesema "Kwa kuwa ni mara yangu ya pili,nataraji ibada hii nitaaifanya vizuri zaidi,kwani mara ya kwanza nilikuwa ni mgeni wa mambo mengi"mwisho wa kumnukuu.

Taasisi ya Tanzania Muslim Hajj Trust itawasafirisha mahujaji wake kwa makundi mawili,ambapo kundi la kwanza linaondoka saa tisa usiku wa leo na kundi la pili litaondoka usiku wa kuamkia tarehe 7 october.

Munira blog inawatakia safari njema na Hijja mabruor.

HAPA WAUMINI WANASOMA DUA KWA AJILI YA KUANZA HAFLA YA KUWAAGA MAHUJAJI.

 RAIS MSTAAFU WA AWAMU YA PILI MZEE ALLY HASSAN MWINYI AKIHUTUBIA LEO KATIKA UKUMBI WA STARLIGHT HOTEL.

KATIBU MKUU  WA TANZANIA MUSLIM HAJJ TRUST SHEIKH ABDALLAH JABIR AKIZUNGUMZA.

 
BAADHI YA AKINA MAMA AMBAO NAO NI MIONGONI MWA MAHUJAJI WAKIWA KATIKA HAFLA FUPI YA KUAGWA.
USTAADH ABDUSHAKUOR KUTOKA DODOMA
MSTAHIKI MEYA WA MANISPAA YA MTWARA MJINI SULEIMAN AHMAD MTALIKA,WAKATI AKIONGEA NA MUNIRA BLOG


KUNDI LA FIRQATU SALAAM,LIKITUMBUIZA.


0 comments:

Post a Comment