Sep 27, 2013

Mfumo wa Elimu walalamikiwa


MFUMO wa elimu nchini unawafanya Watanzania kuwa wageni na nchi yao kwa kutawaliwa na mazingira badala ya kuyatawala kutokana na hali ya maisha ilivyo sasa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) Dk. Jason Ishengoma alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam juzi, alipokuwa akichangia katika mdahalo uliohusu namna ya kuboresha mfumo wa elimu nchini ili uwawezeshe Watanzania kujiajiri na kuajiriwa.

Dk. Ishengoma alisema hali hiyo imezikuta nchi nyingi za Afrika ambazo zimetawaliwa na wakoloni ambao waliamini kutumikiwa ndiyo kufanya kazi badala ya mtu kufanya shughuli zake.
Alisema kutokana na hali hiyo, hata siku moja mfumo wa elimu wa Tanzania na nchi za Afrika zilizotawaliwa na wakoloni haumwezeshi mtu kujitathmini, kujifundisha, kujihoji na kujieleza.
Naye Ofisa Habari na Utetezi wa HakiElimu, Anastazia Rugaba, alisema umefika wakati kwa serikali kubadilisha na kuboresha mfumo mzima wa elimu.
Alisema katika mabadiliko hayo, serikali inatakiwa kuwashirikisha wadau wote wa elimu wakiwamo wazazi na walimu, ili kuwapa fursa ya kutengeneza sera nzuri.
Pamoja na hilo, alizishauru familia kumuandaa mtoto kabla hajazaliwa kwa mama kula vyakula vitakavyomjenga mtoto kiakili na baada ya kuzaliwa kumwandalia elimu yake.

0 comments:

Post a Comment