Ibrahim Boubacar Keita ameibuka mshindi wa uchaguzi mkuu
nchini Mali
huku mpinzani wake akikubali kushindwa katika duru ya pili ya uchaguzi wa
urais.
Soumaila Cisse,amekubali kushindwa na mpinzani wake,aliyekuwa waziri mkuu
Ibrahim Boubakar Keita.
Bwana Cisse aliyewahi kuhudumu kama waziri
wa fedha amempongeza Keita kwa ushindi huo na kumtakia kila la kheri.
Bwana Keita, mwenye umri wa miaka 68, alihudumu kama
waziri mkuu kutoka mwaka 1994 hadi 2000.
Mali
imekumbwa na vurugu kwa kipindi cha mwaka mmoja ikiwemo mapinduzi ya kijeshi na
kufuatiwa na harakati za jeshi la Ufaransa kuwaondoa wapiganaji waliokuwa
wameteka eneo la Kaskazini mwa nchi.
Hata hivyo hakuna matokeo rasmi yametolewa kufuatia duru ya pili ya uchaguzi
iliyofanyika Jumapili.
Katika duru ya kwanza bwana Cisse alipata 19% dhidi ya bwana Keita aliyepata
40%
Bwana Keita anayejulikana kama (IBK) - atakuwa na jukumu la kusimamia zaidi
ya dola bilioni 4 za msaada wa kigeni kwa taifa hilo ambalo uliahidiwa kwa ukarabati wa nchi.
Umoja wa mataifa umeanza kupeleka kikosi cha wanajeshi 12,600 kitakachokuwa
na jukumu la kudhibiti hali nchini Mali, huku wanajeshi wa Ufaransa
wakianza kuondoka.
Baada ya duru ya kwanza ya uchaguzi Bwana Cisse alikuwa amelalamika kuwepo
visa vya rushwa au ununuzi wa kura huku kura zaidi ya laki nne zikisemekana
kuharibika.
Hata hivyo, mahakama ya kikatiba ya Mali ilikataa madai hayo huku
kiongozi wa waangalizi wa Ulaya Louis Michel, akisifu uchaguzi huo kwa
ulivyoandeshwa kwa njia ya uwazi.
Mnamo Jumatatu, waangalizi kutoka Muungano wa ulaya na muungano wa Afrika,
walisifu ambavyo duru ya pili ya uchaguzi ilivyoendeshwa.
'Raia wa Mali
wanapaswa kupongezwa kwa sababu kulingana na mimi ninavyoona, wanatii
demokrasia,'' alisema Michel.
Kabla ya uchaguzi huo Bwana keita aliahidi kuleta maridhiano nchini humo
iwapo angechaguliwa.